Kerala: idadi ya watu waliofariki kutokana na mvua kubwa yafikia ishirini na wawili. 

Katika jimbo la Kerala, idadi ya vifo kutokana na mvua kubwa inayonyesha katika jimbo hilo na maporomoko ya ardhi imefikia watu ishirini na wawili. Mvua hiyo inayonyesha pasi kusita imesababisha uharibifu mkubwa katika jimbo hilo, huku wilaya za Kaskazini zikiathirika zaidi. Huku kiwango cha maji kwenye mabwawa kikifikia viwango vya juu kabisa, mifereji ya mabwawa ishirini na mawili imefunguliwa ili kuondoa maji yaliyozidi. Vikosi viwili vya kukabiliana na majanga pamoja na jeshi vinahusika katika oparesheni za uokoaji.

Habari kutoka kwa ofisi ya kukabiliana na majanga zinasema kuwa watu kumi na mmoja walikufa kutokana na maporomoko ya udongo katika eneo la Idukki, huku wengine watano wakiwa hawajulikani walipo. Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa jimbo hilo Pinarayi Vijayan aliandaa mkutano wa kutathmini hali ilivyo. Kiongozi huyo aliambia vyombo vya habari kuwa hali ni mbaya na kuongeza kwamba mikakati imewekwa ili kukabiliana na hali hiyo.